Swahili   |   English




NOTISI YA KUSUDIO LA KUZIFUTA TAASISI/ ASASI 76
Date: 22 July, 2015 Author: Jafari Malema

Kaimu Mtendaji Mkuu wa RITA Bi Emmy Hudson ( katikati) akizungumza na waandishi wa Habari hii leo katika ukumbi wa mikutano RITA Makao Makuu kuhusu Notisi ya kusudio la kuzifuta Taasisi mbalimbali zilizokiuka taratibu za usajili wa wadhamini, kulia kwak

 

 

TAARIFA KWA UMMA

 

 

 

NOTISI YA KUSUDIO LA KUZIFUTA TAASISI/ ASASI 76

 

 

 

RITA ni Wakala wa Serikali chini ya Wizara ya Katiba na Sheria ambayo pamoja na majukumu mengine imepewa dhamana kusajili Miunganisho ya wadhamini wa Taasisi nchini. Muunganisho wa Wadhamini ni utaratibu unaohusisha usajili wadhamini unaowezesha wadhamini wa Taasisi  kuwa na utu wa kisheria, kuweza kushitaki au kushitakiwakwa jina lake, kumiliki na kuuza mali. Mfumo huu wa Usajili wa Taasisi unaongozwa na Sheria ya Muunganisho wa Wadhamini Sura ya 318, toleo la 2002. (The Trustees’Incorporation Act ,CAP. 318 R.E.2002).

 

Kwa mujibu wa Sheria, Majukumu ya Wadhamini ni pamoja na kuwasilisha marejesho kila baada ya Miezi 12( mwaka mmoja), Kumuarifu Msimamizi Mkuu wa Wadhamini mabadiliko yoyote ya wadhamini (jina la Taasisi,anuani, katiba,kukoma kwa wadhamini kwa sababu yoyote kwa mujibu wa katiba) ndani ya mwezi mmoja baada ya mabadiliko kufanyika, kujua rasilimali na madeni ya Taasisi pamoja na taarifa za kaguzi za hesabu za taasisi, n.k. Msimamizi Mkuu wa Wadhamini anayo mamlaka ya kuzifuta taasisi/asasi ambazo wadhamini wake wameshindwa kutimiza moja ya majukumu yao.

 

Mpaka sasa zipo taasisi 5165 zilizosajiliwa na RITA. Taasisi hizi ni pamoja na Taasisi na madhehebu ya kidini, Vilabu vya michezo, vyama vya Siasa na taasisi binafsi.

 

Kufanya marejesho ya Wadhamini kila mwaka ni utaratibu uliowekwa ili kuonyesha Uhai wa Taasisi na wadhamini wake na pia kama wanatekeleza majukumu yao kama waliovyoainisha katika Katiba zao walizoziwasilisha wakati wanasajiliwa RITA. Zipo taasisi ambazo zimekuwa zikikiuka utaratibu huu. Mwishoni mwa mwaka 2014 RITA kupitia vyombo vya habari  ilichukua jukumu la kuwakumbusha wadhamini kufanya marejesho kama sheria inavyoagiza na kuahidi kufanya uchambuzi na Taasisi zitakazobainika kutotii agizo kufutwa.

 

Awamu ya kwanza ya uchambuzi taarifa imekamilika na taasisi 76 zinakusudiwa kufutwa kama hazitatoa ufafanuzi wa kuridhisha ndani ya Siku 30. Kati ya taasisi hizo zipo 49 za Dar es Salaam na zinazobaki ni kutoka Mikoa mbalimbali  nchini. Pia kati ya hizo 29 ni za kidini na zilizobaki ni za kijamii. Orodha ya Taasisi hizo inapatikana katika Tovuti ya RITA na  matangazo katika Magazeti.

 

RITA inachukua nafasi hii kuzikumbusha taasisi ambazo hazijafanya Marejesho na hazijatajwa katika orodha hii kufanya marejesho haraka vilevile ambazo hazijawasilisha mahesabu yake ya mwaka kufanya hivyo kabla hatua ya kuzifuta hazijachukuliwa.