Description:
KIKAO CHA TATHMINI YA USAJILI WA WATOTO WA UMRI CHINI YA MIAKA MITANO- TABORAMkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Dkt. Batilda Buriani ameongoza Kikao cha Tathmini ya Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri chini ya Miaka Mitano ulioanza kutekelezwa mkoani Tabora Mwezi June 2022. Katika hotuba yake Dkt. Buriani amesema kwamba Usajili kupitia mpango huu umeweza kuongeza kiwango cha Usajii wa Watoto kwa Mkoa wa Tabora kutoka asilimia 9 mpaka asilimia 49 hivyo kuna ongezeko la asilimia 40. Ameongeza kwamba Mkoa utahakikisha kwamba watoto wote ambao hawajapata huduma wanasajiliwa kwani ni haki yao ya Msingi ya Kutambuliwa na kuwataka Wasajili wasaidizi wote waendelee kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu ili kuhakikisha watoto wanaopata vyeti vya kuzaliwa ni wale tu wanaostahili.Akiwasilisha salamu za Wizara ya Katiba na Sheria, Katibu Mkuu Bi. Mary Makondo amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa lengo la kuleta maboresho ya mfumo wa usajili kupitia Mkakati wa Kitaifa wa Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu na Takwimu na kuongeza kwamba Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri chini ya Miaka Mitano ni uthibitisho wa sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha watoto wanasajiliwa na kupata nyaraka ya awali na ya msingi ya utambulisho ambayo ni cheti cha kuzaliwa.Naye Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA Bi. Angela Anatory ameeleza kwamba Mpaka sasa Mpango huu unatekelezwa katika mikoa 23 ya Tanzania Bara ambapo zaidi ya watoto 8,106,469 wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa hivyo kuongeza kiwango cha usajili wa watoto nchini kutoka asilimia 13 na kufikia asilimia 65 hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya mfano katika kuleta mageuzi makubwa katika usajili barani Afrika. Ameongeza kwamba anatoa shukrani kwa Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa, viongozi na watendaji wote kwa ushirikiano ambao wametoa kwa Wakala na wadau wengine kuanzia hatua za mwanzo za maandalizi mpaka kufikia hatua hii.