Swahili   |   English
Gallery : Photo
Album:           SIKU YA WAJANE MKOANI KAGERA

Description: WANANCHI MKOANI KAGERA WAMETAKIWA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUMALIZA MIGOGORO YA MIRATHI Kukosekana kwa uadilifu na mila potofu katika jamii kumechangia kuongezeka kwa matukio ya wajane kuporwa mali, kunyanyaswa, kuteswa na baadhi yao kupoteza maisha na kusababisha watoto walioachwa na marehemu kukosa malezi bora na hivyo kuamua kukimbia mitaani na kuwa omba omba. Hayo yameelezwa hii leo na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Meja Jenerali Charles Mbuge wakati wa mafunzo maalum yaliyokwenda sambamba na maadhimisho ya siku ya wajane Duniani kwa lengo la kuwajengea uwezo Makatibu Tawala wa Wilaya na Maafisa Tarafa wa Mikoa ya Kigoma na Kagera kuhusu kuandika na kuhifadhi wosia, usimamizi wa mirathi pamoja na huduma nyingine zinazotolewa na RITA. Kwa upande wa maadhimisho ya siku ya wajane yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Uhuru Platform Katibu Tawala wa Mkoa huo Prof.Faustin Kamuzora akiwasilisha hotuba kwa niaba ya Mhe. Mkuu wa Mkoa amewaagiza viongozi kupitia ngazi zote kuhakikisha wanatafuta ufumbuzi wa haraka kuhusu kuongezeka kwa migogoro ya mirathi inayosababishwa kwa makusudi na baadhi ya wanandugu kwa makusudi. "Nawaagiza viongozi wa Mkoa kuanzia vitongoji, Vijiji,Kata na Wilaya kushughulikia na kumaliza migogoro ya mirathi inayosababishwa na ndugu wa marehemu wenye nia mbaya na kukosa huruma na hivyo kuwasababishia wajane na watoto kuishi kwa kutangatanga kwa kukosa msaada wa huduma mbalimbali zikiwemo malazi, chakula, mavazi na watoto kuacha shule".Alisema Prof. Kamuzora Naye mwakilishi wa Wajane Mkoa wa Kagera, Bi.Winifrida James Rwezaula alisema kupitia risala yake kuwa wajane wengi wanakosa ushirikiano mzuri kutoka katika vyombo mbalimbali vya maamuzi kuanzia ngazi za chini kabisa za serikali na hiyo ni kutokana na kwamba kundi hilo la wajane kutokutiliwa mkazo stahiki. Bi.Winfrida ametoa ombi kwa serikali kutambua rasmi kuwepo kwa wajane katika jamii ya watanzania na kuandaa mikakati ya kuwahusisha katika kila ngazi ya maamuzi kuanzia serikali ya kijiji, mtaa hadi serikali kuu. Kwa upande wake Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu Bi. Emmy Hudson amesema kuwa RITA ilianzisha huduma ya kuandika na kutunza wosia hasa baada ya kuona mashauri ya mirathi yanaongezeka kwa kasi na kuchukua muda mrefu kukamilika na warithi kuchelewa kupata haki zao. Bi Hudson ameongeza kuwa Wajane ni wadau muhimu kutokana na huduma mbalimbali zinazotolewa na RITA kuwagusa moja kwa moja katika maisha yao ya kila siku, kama vile kusajili na kupata vyeti vya kuzaliwa na vifo pamoja na huduma za usimamizi wa mirathi. ‘’Pia nichukue nafasi hii kutoa wito kwa jamii kuacha kuogopa kwa kuamini mila potofu kwamba kuandika Wosia ni uchuro, imani hiyo si kweli kwani mpaka sasa tumeandika na kutunza wosia 790 kati ya hizo zilizochukuliwa ni wosia 50 na kusimamia mashauri ya mirathi 112.’’Alisema Bi Hudson. Katika maadhimisho ya mwaka huu RITA inashiriki kwenye Viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es salaam na Mkoani Kagera kwa kutoa elimu na msaada wa kisheria bure kuhusu kuandika na kuhifadhi wosia na usimamizi wa mirathi.

Album Pictures