RITA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini
`
Ufilisi watu Binafsi
FRANK KANYUSI FRANK
Administrator General And Chief Executive Officer

NINI MAANA YA UFILISI?


Ufilisi ni hali ya mtu binafsi au taasisi kushindwa au kutokuwa na uwezo wa kulipa madeni na kuendesha shughuli za biashara. Katika kuhakikisha kuwa watu binafsi au taasisi hazifikii hali ya ufilisi sheria zimeweka mifumo mbalimbali ya kuchukua hatua za kurekebisha taratibu za uendeshaji wa biashara ili kupunguza athari endapo mtu binafsi au taasisi itafikia hali ya kusitisha shughuli zake.


Ufilisi ni utaratibu wa kisheria unaomwezesha mtu au kampuni ambaye/o imefilisika kumalizana na wadeni wake kwa mali zake kuwekwa chini ya usimamizi wa mfilisi atakayeziuza na kulipa madeni yote au sehemu yake kama kiasi kinachopatikana hakitoshi. 


Wakala hutoa huduma za ufilisi wa watu binafsi na ufilisi wa makampuni. Taratibu za Ufilisi zimeelezwa katika Sheria ya Ufilisi Sura ya 25 ya Sheria za Tanzania Bara na Sheria ya Makampuni Sura ya 212 pamoja na kanuni zake. Mahakama Kuu ndiyo pekee yenye mamlaka ya kusikiliza mashauri ya ufilisi. Ofisi ya kabidhi Wasii Mkuu husimamia masuala ya Ufilisi wa kampuni baada ya kuteuliwa na mahakama kulingana na hali ya kampuni ilivyo kabla ya kufikia hatua ya kufilisika  Kwa mujibu wa Sheria ya Ufilisi Sura ya 25 Kabidhi Wasii Mkuu ni Mpokezi Rasmi na hutekeleza majukumu yafuatayo kuhusiana na mwenendo wa mdaiwa:

 

a)    Kuchunguza mwenendo wa mdaiwa na kutaarifu mahakama, kueleza ikiwa kuna sababu ya kuaminika kwamba mdaiwa ametenda kitendo chochote ambacho ni kosa chini ya Sheria hii, au sheria yoyote iliyofutwa na Sheria hii, au ambayo inaweza kuhalalisha mahakama kukataa, kusimamisha au kustahilisha amri ya kuondolewa kwake;

b)    Atoe taarifa zingine zinazohusiana na mwenendo wa mdaiwa kwa mujibu wa   maelekezo ya mahakama;

c)      Kushiriki katika uchunguzi wa mdaiwa kadri atakavyoona inafaa;

d)    Kushiriki na kusaidia kuhusiana na mashtaka ya deni lolote la ulaghai kadri Mwanasheria Mkuu atakavyoelekeza.

Vilevile, kuhusiana na mali za mdaiwa Mpokezi rasmi pamoja na majukumu mengine ana  majukumu yafuatayo: -

a)    Kuwa mpokezi wa muda wa mali ya mdaiwa ambapo meneja maalum huteuliwa akisubiri uteuzi wa mdhamini;

b)    Kumwelekeza meneja maalum kutafuta vyanzo mbalimbali vya fedha ikiwemo kukopa kwa maslahi ya wadai au kadri itakavyofaa;

c)     Kuitisha na kuongoza mkutano wa kwanza wa wadai;

d)    Kutoa fomu za wawakilishi kwenye mikutano ya wadai;

e)    Kuwataarifu wadai kuhusu pendekezo lolote ambalo mdaiwa anaweza kuwa ametoa kuhusiana na njia ya kufilisi mali zake;

f)      Kutangaza amri ya kupokea, tarehe ya mkutano wa kwanza wa wadai, na uchunguzi wa wazi wa mdaiwa, na mambo mengine ambayo yatahitajika kutangazwa;

g)    Kuwa mdhamini wakati wowote nafasi hiyo ikiwa wazi katika ofisi ya mdhamini

UFAFANUZI WA ZIADA

Ombi la mdaiwa

  • Mdaiwa atawasilisha taarifa kuhusu mali zake Mpokeaji Rasmi kabla ya kufungua Ombi mahakamani.
  • Mpokeaji Rasmi atatoa hati ya kukiri kupokea na kuiwakilisha Mahakamani.
  • Mahakama ikiridhika itatoa amri ya Upokeaji na Mpokeaji Rasmi anakuwa Mpokeaji aliyeteuliwa.
  • Mpokeaji Rasmi ataendelea chini yaSheria ya Ufilisi, Sura ya 25 Toleo la 2002 na kufilisi mali ya mdaiwa.


Ombi la Mdai

  • Mdai atafungua ombi mahakamani kupata amri ya kufilisi mali ya mdaiwa.
  • Mpokeaji Rasmi atatoa hati na kuwasilisha mahakamani.
  • Mahakama itatoa amri ya Upokeaji na Mpokeaji Rasmi anateuliwa kuwa Mpokeaji.
  • Mpokeaji Rasmi ataendelea chini ya Sheria ya Ufilisi, Sura ya 25 toleo la 2002 na Kanuni zake kufilisi mali ya mdaiwa.
Ona Ukurasa Kamili
Washirika wetu
Wadau Wetu