Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt. Damas Ndumbaro
amewaonya baadhi ya viongozi wa Bodi za wadhamini wa taasisi za kidini, vyama
vya siasa na vyama vya michezo kwa ubadhirifu na matumizi mabaya na
kujimilikisha mali za taasisi hizo kinyume na sheria.
Hayo ameyasema leo Machi 13, 2025 wakati wa mkutano wa wajumbe wa bodi za
wadhamini zilizomo Mkoa wa Dar es Salaam uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa
wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere.
“Sisi sote ni mashahidi wa ongezeko la migogoro katika taasisi mbalimbali
nchini ambayo inasababishwa na mapungufu ya usimamizi wa majukumu ya bodi za
wadhamini. Inashangaza kuona hali hii inajitokeza hata katika taasisi za kidini
ambazo kikawaida zinatakiwa kuwa mfano wa kuigwa katika jamii,” amesema Dkt.
Ndumbaro.
Pia, amebainisha kuwa, migogoro katika taasisi na jamii inatokana na baadhi ya
wadhamini kufuja fedha na kutumia hovyo mali za taasisi hususani ubadhirifu wa
fedha.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa RITA Dkt. Amina
Msengwa amewataka wajumbe wa bodi za wadhamini kuheshimu Sheria na katiba zao
kwani zimebainisha ukomo wa uongozi wao, ufanyaji wa maamuzi na usimamizi wa
mali za taasisi na kutambua kuwa wao siyo wamiliki wa mali hizo bali ni
wasimamizi tu.
Naye Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA Bw. Frank Kanyusi
amesema kuwa kikao hicho ni muendelezo wa mikakati yao ya kukutana na wadau ili
kwa pamoja waweze kutatua changamoto za uendeshaji na usimamizi wa mali za
waumini au wanachama wao kwa maslahi mapana ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Tags : #Insolvency