Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) leo Machi 25, 2025 umewasilisha taarifa ya utekelezaji na usimamizi wa Bodi za Wadhamini wa Taasisi za Kidini, vyama vya Siasa, vyama vya Michezo na taasisi za kijamii kwa Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria jijini Dodoma.
Akitoa maelezo kwa Kamati hiyo, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema kuwa hivi karibuni alitoa maagizo kwa Bodi zote za Wadhamini kujisajili kidijitali, kuhuisha katiba zao, kuwasilisha marejesho kwa wakati pamoja na kufanya uchaguzi wa Wajumbe wa Bodi za Wadhamini.
Pia, Mhe. Waziri alieleza kamati hatua zilizochukuliwa na RITA kwa Bodi za Wadhamini ambazo zilibainika kufanya ubadhirifu wa mali na kusababisha migogoro ya mara kwa mara.
" Mhe. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, RITA iliwaondoa wajumbe wa Bodi za Wadhamini wa Taasisi za Kidini waliobainika kuganya ubadhirifu na kuchochea migogoro na kuunda Kamati maalum za uchunguzi, pia inaendelea kufuatilia na kutatua migogoro katika taasisi hizo zenye Bodi za Wadhamini". Alisema Mhe. Dkt. Ndumbaro.
Tags : #Trusteeship