RITA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini
MEDIA CENTRE
August
10
2025
''RITA ENDELEENI KUWEKEZA ZAIDI KWENYE MIFUMO YA KIDIJITALI''. MASWI
News & Update
JAFARI MALEMA
`

Katibu Mkuu wa Katiba na sheria Bw. Eliakim Maswi ameitaka RITA  kuendelea kuwekeza kwenye mifumo ya kidigitali, kuhamasisha wananchi, na kuhakikisha kuwa huduma za usajili wa matukio Muhimu ya Binadamu kwa njia ya kidijitali inamfikia kila mtu – bila kujali anaishi wapi au ana hali gani ya kiuchumi.

Ameyasema hayo katika hafla ya kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu Barani Afrika ambayo yanafanyika kila mwaka Tarehe 8 Agosti na kitaifa mwaka huu kuadhimishwa Mkoani Dodoma yakiwa na kauli mbiu ya Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni; “Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu ni Msingi wa Miundombinu ya Kidijitali ya Umma na Mifumo ya kidijitali ya Utambuzi wa Kisheria Barani Afrika”.

Amesema kwamba Dunia ya leo inaendeshwa na teknolojia na Tanzania haiwezi kubaki nyuma. Usajili wa matukio muhimu kwa njia ya kidigitali unaleta manufaa makubwa ikiwa pamoja na Usahihi na uharaka wa taarifa, upatikanaji rahisi wa taarifa za wananchi, kuwezesha uunganishaji wa mifumo ya kitaifa kama vile NIDA, mfumo wa afya, elimu na kuhakikisha Usalama wa taarifa kwa kutumia teknolojia za kisasa za usimbaji na uthibitisho wa utambulisho.

Kwa kupitia mpango wa Digital CRVS System uliozinduliwa 2022, zaidi ya kumbukumbu milioni 3 zimeingizwa katika mfumo wa kidigitali, zikiwa salama na zenye upatikanaji wa haraka. Mafanikio haya mafanikio yanatokana na uwekezaji katika miundombinu ya TEHAMA, mafunzo ya watumishi, na uhamasishaji wa wananchi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

“Usajili wa matukio muhimu ya binadamu ni urithi wa kitaifa ni alama ya heshima kwa kila raia na ni injini ya maendeleo ya taifa. Bila takwimu sahihi, hatuwezi kupanga vizuri, kufuatilia maendeleo, au kutathmini changamoto zinazotukabili.’' Amesema Bw. Maswi.

Ametoa wito kwa serikali za mitaa, sekta binafsi, asasi za kiraia, na washirika wa maendeleo kuendelea kushirikiana na RITA ili kuhakikisha kuwa kila tukio la kizazi, ndoa, talaka, na kifo linarekodiwa na kuhifadhiwa kwa njia ya kidigitali ambayo inahakikisha usahihi na  usalama wa taarifa.

Akitoa maelezo ya awali kuhusu hafla hiyo, Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA Bw. Frank Kanyusi ameeleza kwamba maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika kwa mara ya 8 tangu kuanzishwa kwake 2018 lengo lake kuu likiwa kuongeza mwamko na kasi ya wananchi kusajili matukio ya vizazi, vifo, ndoa, talaka na Watoto wa kuasili mara tu yanapotokea.

“RITA kama taasisi iliyo na jukumu la kusimamia na kuratibu usajili wa matukio haya hapa nchini tumekuwa na mikakati na program mbalimbali za kuhakikisha tunaongeza kasi ya usajili wa matukio haya hapa nchini ambayo nguzo na msingi wake mkuu ni matumizi ya mifumo ya kidijitaki”. Amesema Bw. Kanyusi.

Ameongeza kwamba Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inasisitiza kuongeza matumizi ya TEHAMA kwa ajili ya kuongeza kasi ya  Usajili wa Matukio muhimu ya Binadamu na kwamba kwa kupitia mfumo wa eRITA, wananchi sasa wanatuma maombi huduma hizo bila kufika Ofisi za Wakala na kuchagua Wilaya iliyo karibu na mwombaji kwa ajili ya kuchukua cheti cha huduma aliyoomba kwa wakati.

 

 

 

 

Â