Description:
Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) umetoa elimu kwa wajane kuhusu kuandika na kuhifadhi wosia pamoja na msaada wa kisheria kuhusu suala la usimamizi wa mirathi. Akizungumza na Wajane hii leo jijini Dar es salaam katika semina maalum ya siku moja, Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu Bi Emmy K. Hudson amewataka wajane kutokata tamaa kutokana na migogoro ya kugombania Mali zinazoachwa na waume zao kutoka kwa ndugu wa marehemu badala yake watulie na kufuata taratibu za kisheria ili kumaliza matatizo yanayowakabili, " najua mnanyanyasika, mnateseka lakini niwahakikishie kwamba RITA ni Taasisi ya Serikali ipo itawasaidia ili haki itendeke na muweze kurudi katika hali zenu za kawaida za uzalishaji mali na kulijenga Taifa badala ya kuendelea kuishi kwa majonzi na kukata tamaa."Alisema Bi Hudson. Siku ya wajane duniani huadhimishwa kila inapofika tarehe 23 Juni ambapo nchini Tanzania kitaifa maadhimisho hayo yalifanyika mkoani Dodoma na mgeni rasmi alikuwa ni Waziri wa Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Mhe.Ummy Mwalimu.