BRS itaweza kuhakikisha kuwa watoto wote wachanga wanaozailiwa husajiliwa katika kipindi cha siku 90 baada ya kuzaliwa, ni lazima pia iwezeshe, wakati wote wa maisha yao, usajili wa idadi kubwa ya watu ambao kuzaliwa kwao hakukusajiliwa . Vifaa vya ukusanyaji taarifa na takwimu vya kisasa zaidi na mfumo ya mawasiliano vitatumika kujenga mfumo wa BRS wenye ubunifu na ufanisi. Katikati yake kutakuwa na kituo cha data salama kinachoingizwa taarifa mpya kila mara, ambacho kitatoa na kuhifadhi data kwa ajili ya mchakato wa usajili na kutegemea mahitaji/masharti ya usalama na uaminifu kutimizwa, kwa mashirika mengine ya Serikali.
UZINDUZI WA UFUMO WA BRS4G JIJINI DODOMA
‘’WANANCHI CHANGAMKIENI FURSA YA USAJILI WA VYETI VYA KUZALIWA’’
Wananchi wametakiwa kuhakikisha wanawasajili Watoto na kupata vyeti vya kuzaliwa mapema mara baada ya kuzaliwa ambacho kitawawezesha kupata huduma mbalimbali za jamii zikiwemo elimu, Bima ya Afya, ajira, pamoja na pasi za kusafiria ng’ambo ya Nchi.
Wito huo umetolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa tarehe 23 Juni 2018 Jijini Dodoma wakati kilele cha maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma na uzinduzi wa mifumo ya utoaji huduma kwa njia ya kielekroniki kwa Wizara na Taasisi za Serikali.
Mhe Majaliwa ameongeza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kusajili matukio hayo ya vizazi, vifo ndoa na talaka kwa kuwa ndiyo sehemu pekee inayowezesha kupata takwimu muhimu na sahihi zitakazosaidia katika kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo.
‘’Natambua na nimeona kazi nzuri inayofanywa na RITA hapa uwanjani kwani wananchi wanahudumiwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa na vifo bila usumbufu wala rushwa hivyo kuthibitisha mifumo hii ninayoizindua leo inaongeza uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa Wananchi’’.
Kwa upande wake Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt, (MST) George Mkuchika amesema kuwa kwa muda mrefu Serikali imeendelea kutambua umuhimu wa kuboresha huduma zake kwa umma kupitia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kuzingatia Mipango ya Taifa ya Maendeleo ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 -2015-2016) ambayo inasisitiza matumizi ya TEHAMA katika kukuza uchumi.
Waziri Mkuchika amefafanua kuwa Mfumo wa wa utoaji huduma za Usajili wa Vizazi kutumia TEHAMA umeanza kufanya kazi kwenye vituo 60 katika Mikoa mitatu ya Geita,Shinyanga na Dar es salaam,ambapo jumla ya Wilaya 13 kata 6 Hospitali 20 na Vituo vya Afya 21 na ufumo umeonesha ufanisi mkubwa katika utoaji wa huduma.
Ameongeza kuwa ili kuiwezesha mifumo iliyozinduliwa kuwafikia wananchi wengi Nchini, Serikali imeweza kupanua wigo wa matumizi ya TEHAMA hadi maeneo ya Vijijini kwa kuzipatia ruzuku kampuni za simu ambazo ni Airtel Tanzania Limited,Vodacom Tanzania Limited, MIC Tanzania Limited pamoja na Shirika la simu Tanzania (TTCL) ambapo jumla ya kata 286 za vijijini zenye jumla ya vijiji 1279 kati ya kata 347 zenye jumla ya Vijiji 1393 zimefikiwa na huduma za mawasiliano hadi kufikia mwishoni mwaka jana.
‘’ Mfumo wa kuandikisha Vizazi na vifo (Birth and Dearth Ragistration System) utawezesha kuongeza tija na ufanisi wakati wa kuandikisha taarifa za vizazi na vifo hapa Nchini’’.
Akitoa maelezo kuhusu huduma za usajili wa vizazi na vifo, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya RITA Prof Hamis Dihenga amesema kuwa usajili wa matukio muhimu ya Binadamu na Takwimu (vizazi,vifo, ndoa na talaka na watoto wa kuasili) unapaswa kutiliwa mkazo kwa kuwa ndiyo chanzo cha kupata taarifa sahihi za matukio hayo ambapo itasaidia katika kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo.
Dihenga ameendelea kusema kuwa RITA inahitaji rasilimali watu na fedha ili kuhakikisha inakuwa na uwezo wa kuwafikia na kutoa huduma kwa wananchi wengi hasa wale wanaoishi vijijini ambao kwa kiasi kikubwa wanashindwa kupata huduma hii kutokana na changamoto mbalimbali.
‘’ Kama tunavyoona hii leo tunazindua mfumo huu wa usajili wa vizazi na vifo na wananchi wamejitokeza na wamefurahia huduma ya usajili wa vizazi na vifo kwa kuwa wanasajiliwa na kupatiwa vyeti papo hapo’’.
Mifumo iliyozinduliwa ni ile iliyojengwa kupitia miradi iliyogharamiwa na Serikali na Washirika wa Maendeleo wa Kimataifa na inawezeshwa kufanya kazi na kutoa huduma kupitia Miundombinu ya Mawasiliano ya Serikali ( Government Communications Network- GovNet) na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (National ICT Communication Broadband Backbone – NICTBB).