Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) umezindua na kutekeleza Mpango Mkakati wa Usajili na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa Watoto wa umri Chini ya miaka mitano. Mpango huu umeboreshwa na kuondoa changamoto zilizokuwepo hapo awali zilizosababisha watoto wengi wanaozaliwa kutosajiliwa, mfano umbali kutoka ofisi za Wakuu wa Wilaya na wanakoishi wananchi pamoja na ada ya kupatiwa huduma, kutokana na maboresho yaliyofanyika katika mpango huu yamewezesha kuongeza idadi ya Usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wa kundi hilo na hasa pale tukio linapotokea aidha katika kituo cha tiba kinachotoa huduma ya mama na mtoto au nyumbani ( kwa Mkunga wa jadi), sambamba na kuboresha mfumo huo wa usajili, pia Mpango huu umelenga kugatua na kukasimusha majukumu kutoka Serikali kuu na kuhamia Serikali za Mitaa, hii inamaana kwamba hapo awali shughuli za usajili zilikuwa zikisimamiwa pekee na ofisi ya Mkuu wa Wilaya kama jukumu la kisheria ambapo Katibu Tawala wa Wilaya ndiye msajili kwa niaba ya kabidhi Wasii Mkuu.
Mpango wa usajili na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa watoto wa umri chini ya miaka mitano unatekelezwa na RITA kwa kushirikiana na wakurugezi wa Halmashauri zote katika kila Mkoa ambao utatekeleza mpango huo, hapa ieleweke kwamba haina maana kuwa ofisi ya Mkuu wa Wilaya haitokuwa na jukumu tena, hapana majukumu mengine ya usajili wa watoto na makundi mengine ya Wananchi waliovuka miaka mitano yanaendelea katika ofisi hizo na Mkuu wa Wilaya ni msimamizi wa shughuli zote za kiserikali katika Halmashauri zote zilizopo katika Wilaya yake likiwemo hili la Usajili wa watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Misingi muhimu ya Mpango huu ni kama ifuatavyo:-
- Kuondoa ada ya huduma, hii inamaana kuwa vyeti hivyo vinatolewa bure.
- Kugatuliwa kwa madaraka kutoka serikali kuu hadi serikali za mtaa ili kuwezesha kusogeza huduma karibu na makazi wanakoishi wananachi, hivyo vituo vya usajili ni ofisi za watendaji kata na vituo vya tiba vinavyotoa huduma ya mama na mtoto.
- Matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano TEHAMA, matumizi ya simu za mkononi katika kusajili na kutuma taarifa zote za usajili kutoka katika kila kituo ambapo zinatumwa moja kwa moja hadi katika kanzi data ya RITA Makao makuu.
Mpango Mkakati huu wa usajili ulizinduliwa katika Mkoa wa Mbeya mnamo mwaka 2013 kisha baadaye kutekelezwa katika Mikoa mingine 20 ya Tanzania Bara ambayo ni Mbeya ,Songwe, Mwanza, Iringa, Njombe, Geita, Shinyanga, Mtwara, Lindi, Mara, Simiyu, Ruvuma, Dodoma, Singida, Morogoro, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
Takwimu za hivi karibuni zinaonesha mafanikio kwa kuongeza idadi ya usajili, kutokana na takwimu za sensa ya makazi na watu ya mwaka 2012 inaonesha wananchi waliosajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa ni asilimia 13 tu, lakini kupita mpango huu jumla ya Watoto 5,939,509 wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa hivyo kuongeza takwimu na kufikia asilimia 55.
RITA inashirikiana na wadau mbalimbali wa Kitaifa na Kimataifa ikiwemo wizara ya katiba na sheria, Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Idara ya uhamiaji, Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa NIDA pamoja na Wadau wa Maendeleo ambao ni Shirika la kimataifa la kuhudumia watoto(UNICEF),shirika la maendeleo la Serikali ya watu wa Canada na Kampuni ya simu za Mkononi TIGO.
Muhimu kuzingatia:-
Kwa Mikoa ambayo inatekeleza mpango huu na ikiwa Mtoto yuko chini ya umri wa miaka mitano cheti atapatiwa bila ya malipo (ni bure) ikitokea mzazi au mlezi amepoteza au kuharibika itampasa kufika katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri anakoishi na atalipia shs.5000/= na kupatiwa cheti kingine kwa taarifa zilezile za awali.
Matukio ya Mkakati wa Usajili wa Watoto chini ya miaka Mitano katika Mikoa 26 . Bofya